Sunday, November 23, 2014

MARI FC MDEBWEDO

Timu ya soka ya Mari Fc. Inayoundwa na wafanyakazi wa kituo cha utafiti wa kilimo kilichopo maeneo ya Mikocheni jana ilikubali kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa mashabiki wa yanga waliopo kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook katika mtanange wa kirafiki uliopigwa kwenye uwanja wa chuo cha Takwimu kilichopo maeneo ya Changanyikeni jijini Dar.


Mashabiki hao wa wana Jangwani ndiyo walikuwa wa kwanza kuandika bao kunako dakika ya 20 ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wao Jumanne juma ambaye aliwahadaa mabeki wawili wa timu ya Mari kabla ya kumlamba chenga na mlinda mlango wao na kisha kupachika bao kirahisi.

Dakika tatu baadaye Yanga walipata bao la pili kupitia kwa mshambuliaji wao hatari Yule Yule Jumanne ambapo alipokea pasi safi kutoka wingi ya kushoto na kuukwamisha mpira ule kimiani kiurahisi huku akimwacha kipa wa Mari Fc akiwa hana la kufanya hivyo mpaka wanakwenda mapumziko Mari ilikuwa nyuma kwa mabao mawili kwa nunge.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikifanya mabadiliko lakini almanusura mabadiliko hayo yawe na faida kwa mali ambao walifanikiwa kusawazisha mabao yote mawili kupitia kwa mshambuliaji wao Zacharia Muyengi lakini hata hivyo udhaifu wa mwamuzi wa mchezo huo Said Komba Minazi uliwafanya Yanga wapate bao la tatu na matokeo kuwa 3-2.

Minazi alitoa adhabu ya penati kutokana na mchezaji wa Yanga kukwatuliwa nje ya eneo la hatari kitu kilicho lalamikiwa mno na wachezaji wa Mari ingawa yote kwa yote refa alibaki kuwa mwamuzi wa mwisho na matokeo yakabaki hivyo mpaka dakika ya mwisho.

Akiongea na blog hii mmoja wa viongozi wa Mari Zacharia Muyengi  alisema mechi  hiyo imewapa changamoto na watayafanyia kazi makosa waliyoyaona ili mechi nyingine waweze kutoka kifua mbele.


“Nashukuru kwamba kocha viongozi wa timu na mzee wa timu kila mmoja ameyaona makosa yapo wapi hivyo tunajipanga kuyarekebisha ili mechi zijazo tuweze kushinda kwani hizi ni mechi za kirafiki kabla ya ile ziara yetu ya Zanzibar.” Alisema Muyengi.

No comments:

Post a Comment

KATUNI ZA MWAGITO HIZI HAPA MWANANGU.