MASHUJAA walioitoa kimasomaso Tanzania kwa
kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga
wanatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, huku
wakisema haikuwa kazi rahisi kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola.
Yanga imesonga mbele baada ya ushindi wa jumla wa
mabao 2-1, ikiwa ni kutokana na kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza jijini Dar
es Salaam, kabla ya kukubali kipigo cha 1-0 ugenini juzi.
Katika mchezo huo wa juzi, wachezaji wa Yanga
walikumbana na changamoto kadhaa kutoka kwa wapinzani wao, wakiwamo waamuzi
walioonekana wazi kuwapendelea wenyeji hao.
Moja ya ‘figisu figisu’ hizo ni kitendo cha nahodha
wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuonyeshwa kadi nyekundu, mshambuliaji Donald
Ngoma kuibiwa vitu vyake na kubwa zaidi ni mwamuzi kuwapa wenyeji penalti
dakika za lala salama ambayo ilipanguliwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Kutokana na ushujaa ulioonyeshwa na Dida kwa kuokoa
adhabu hiyo, mashabiki wa Sagrada walimpiga jiwe, lakini hilo hakikuwasaidia
wenyeji hao kuhimili vishindo vya wakali wa Jangwani, maarufu kwa jina la
Wakimataifa.
Kwa hali ilivyokuwa muda wote wa mchezo huo ikiwamo
waandishi wa habari wa Tanzania kuzuiwa kupiga picha, ni wazi kuwa kupita kwa
Yanga kwenye hatua hiyo ilikuwa ni zaidi ya vita kama alivyokiri kocha mkuu wa
timu hiyo, Hans van der Pluijm, akiungwa mkono na baadhi ya wachezaji wake.
Akizungumza na BINGWA, Pluijm alisema haikua kazi
rahisi kikosi chake kutinga hatua ya makundi kutokana na changamoto mbalimbali
alizokutana nazo, huku akitamba kuwa na imani kubwa ya kufika fainali ya
michuano hiyo.
Hata hivyo, Mholanzi huyo alisema kuwa hakushangazwa
kikosi chake kutinga hatua ya makundi kwani analifahamu vyema soka la Afrika
katika ngazi ya klabu.
“Sishangazwi na hatua hii tuliyofikia ya kuingia
hatua ya makundi ya michuano ya Shirikisho, hii si mara yangu ya kwanza
kuipeleka timu hatua hii, niliwahi kuifikisha hatua kama hii Berekum Chelsea (ya
Ghana) mwaka 2012,” alisema Pluijm.
Alisema vijana wake walipambana na kujitoa muhanga katika
mchezo huo wa juzi licha ya figisu figisu walizokutanazo kuhakikisha
wanaipeperusha vyema Bendera ya Tanzania.
“Nawapongeza vijana wangu, japo tumefungwa bao 1-0,
lakini cha muhimu tumefanikiwa kusonga mbele, ila ni vema tukafahamu bado tuna
safari ndefu zaidi ya mafanikio,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Yanga, Jerry Muro, amesema kuwa kikosi chao kinatua nchini leo saa 8:30 mchana
wakitokea Angola na kwamba kitaenda moja kwa moja kambini kwa ajili ya safari
ya kesho kwenda mjini Songea tayari kwa mechi yao ya mwisho ya Ligi Kuu
Tanzania Bara dhidi ya Majimaji ya huko.
Aliwataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi Uwanja
wa Ndege kuwalaki mashujaa wao watakaotua kwa kutumia ndege ya Shirika la
Afrika Kusini (South African Airways).
Baada ya kutua, mashabiki wataandamana kuisindikiza
timu yao hadi makao makuu yao yaliyopo Mtaa wa Jangwani, huku wakitarajiwa
kuuteka Mtaa za Msimbazi yalipo maskani ya watani wao wa jadi, Simba.
“Bada ya mchezo wetu wa Jumapili dhidi ya
Majimaji, timu itarejea Dar es Salaam Jumatatu kwa ajili ya maandalizi ya
mchezo wetu wa fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (FA) dhidi ya Azam FC
Jumatano ya wiki ijayo,” alisema
No comments:
Post a Comment