NDANI YA MABATINI STADIUM:
Kibaka
asepa na mabovu ya inchaji
“AYAAAA, yule mchizi aliyekuwa amechili benchi lile
yupo wapi?” Waswazi kimya huku wengine wakijitahidi kuvuta kumbukumbu za huyo
anayeuliziwa bila mafanikio.
“Ebwana eeh, kazi ya kutambua watu wanaoingia humu
na kutoka ni ya kwako, kazi yetu sisi ni kukulipa kiingilio na kuangalia ndiki
inavyopigika,” akajibu mswazi mmoja lakini huku jicho lake likiwa tisti kunako
runinga.
“Oya, masela kuweni na busara basi mjue mchizi
kasepa na mabovu yote niliyoyaacha hapa,” alisema Peter.
Mwana huyo ambaye ni inchaji wa kibandaumiza kile na
kuwafanya waswazi wote waliokuwa ndani humo wamgeukie kwa mshangao na jicho la
huruma unajua ilikuwaje?
Wakati waswazi wakiwa wanafuatilia mbugi kideoni
mara nje zikasikika kelele za mwizi, waswazi wote kibandani wakatoka mbio
lakini wakati wengine wakiishia mlangoni na kurudi ndani.
Wenzao
wengine waliunga kumkimbiza kibaka akiwamo inchaji wa sehemu ile ambaye alikuwa
kati ya wale waliokuwa na hamu ya kumkamata mwizi.
Kumbe inchaji huyu wakati akikurupuka na kuanza
kukimbiza mwizi alikiacha kikoba chake ambacho kilikuwa na mabovu aliyotoka
kuwachanja waswazi muda mfupi.
Wakati yupo kwenye purukushani hizo ndipo mmoja wa washkaji waliokuwa karibu na
kikoba hicho alipoamua kujisevia na kusepa zake kimya kimya.
Kwa mujibu wa Peter, kiasi kilichokuwa kikobani ni
shilingi 57,000 ambazo alikuwa amekusanya kutoka kwa waswazi waliokuwa
wakifuatilia ndiki ya Kagera dhidi ya Mnyama ambayo ilimalizika kwa matokeo
kama mlivyoona na kusikia.
Ebwana eeh, hii ngoma ilikuwa ni ndani ya Mabatini
Stadium, hapa naizungumzia mitaa ya Vingunguti, anasimama Joseph Martin kama
mmiliki wa kibanda hiki.
Lakini Peter Muro ndiye inchaji mchanjaji wakati
wote ikipigwa ndiki kubwa na hata ndogo kama hizi bwana mkubwa huyu anasimama
langoni kuwachanja.
Hapa mwanakwetu wanazama waswazi 65 pekee kwa ndiki
za kawaida, lakini siku kikinuka kweli kweli waswazi wanabanana na kufikia 70
ingawa siku nyingine kikinuka zaidi hufikia hadi 75 ingawa hukaa hadi kwa
kubebana.
Kwa mujibu wa inchaji huku pia kuna wakishua ingawa
waswazi ni wengi zaidi, wakishua wa huku siku hizi wanaachana na runinga za
homu na kujichanganya uswazi kupata burudani zinazotokea ndani ya vibandaumiza
na hasa siku zinapopigwa ndiki za majuu.
Buku pekee inatosha kukufanya uone ndiki ndani ya
Mabatini lakini pia unaweza kuagiza kinywaji chochote au fegi ingawa si ruhusa
kuvuta fegi wakati ndiki ikiendelea.
Pande hizi waswazi wanafuatilia zaidi ligi ya
England ikifuatiwa na hii ya madafu ambayo hakukuwa na haja ya kuwa na ratiba.
Maana ligi hii kila uchwao hubadilika hata kwa jambo
lisilo la lazima, ilimradi kinachosimamisha kiwe kinahusu mabovu, ha ha ha
haaaa!!!..hii si ya humu lakini imeingia bahati mbaya tu.
Angalau waswazi wa huku nao wanaanza kupenda ligi ya
Ubelgiji na wanasema mbali na Mbwana Samatta kuwa anacheza huko, lakini kinachowavutia
zaidi wanandinga wa huku ni jinsi anavyozidi kupachika mabao kila uchwao na
kuipeperusha bendera ya nyumbani vyema.
Hata hivyo, unaambiwa ukitoa runinga siku inapopigwa
ndiki yoyote ya Italia utaishia kuhesabu viti hata iwe ni ndiki ya upinzani kiasi
gani waswazi hawatoi hela.
Yaani ni bora uwawekee muvi walipie hata jero lakini
si mechi labda kidogo kwa wazee wa kubeti ndio wanaweza kuangalia ili kuhakiki
mikeka yao.
Ebwanaeeh, hii ni kutoka ndani ya Vingunguti kwenye
Kibandaumiza cha Mabatini, mimi na wewe mkali wangu wa nguvu tugumiane kiswazi
kipandeni hapa wiki ijayo lakini usikose kunialika wikiendi hii kibandani
kwako.
No comments:
Post a Comment