Thursday, June 12, 2014

MMWILI WA GEORGE TYSON HAUJAZIKWA MPAKA LEO :MAZITO YAIBUKA


 
habarika sasa kwamba, mwili wa aliyekuwa mwongoza filamu za Kibongo, marehemu George Otieno Okumu ‘Tyson’ (41) aliyefariki dunia Mei 30, mwaka huu kwa ajali mbaya ya gari nchini Tanzania na kusafirishwa kwao,Kenya bado haujazikwa huku mazito yakiibuka kuhusiana na msiba huo!

 
Mwili wa aliyekuwa mwongoza filamu za Kibongo, marehemu George Otieno Okumu ‘Tyson’ (41) ukiwa kwenye jeneza. Chanzo cha ndani kimeliambia Amani kwamba, mwili huo utazikwa keshokutwa Jumamosi kijijini kwao huko Kisumu baada ya kukaa mochwari kwa siku kumi na nne tangu kifo.
WAOMBOLEZAJI WAENDELEA NA SHUGHULI ZAO
Katika hali ya kushangaza, utamaduni wa Kenya si kama wa Bongo, misiba hupewa kipaumbele siku za mwishoni mwa wiki, hasa Jumamosi.
“Kwa sasa mwili upo mochwari, unasubiri kuzikwa Juni 14 (mwaka huu). Kwa hiyo ukifika kwenye nyumba yenye msiba ambayo ipo Donholm, Phase 5 jijini Nairobi, unaweza kusema hakuna msiba.
Watu wanaendelea na shughuli zao za kila siku, kama kwenda sokoni na sehemu nyinginezo.
“Kifupi huwezi kujua kama kuna msiba. Huu ndiyo utaratibu wetu hapa Kenya, si kama huko Tanzania,” kilisema chanzo hicho.
 
Mwili wa Tyson ukichukuliwa mara baada ya kuagwa tayari kwa safari ya Kenya. Kikaendelea: “Ila Ijumaa ijayo, ndiyo kidogo kutaonesha kama kuna msiba kwani mwili utachukuliwa kwa ajili ya taratibu za kuaga kisha Jumamosi utapelekwa Kisumu, kwenye Kijiji cha Siaya ambako marehemu atazikwa.”
  MONALISA, SONIA WALALA HOTELINI
Habari zaidi zinadai kuwa, baada ya kufika jijini Nairobi na mwili wa marehemu, mtalaka wa marehemu, Yvonne-Cheryl Ngatikwa ‘Monalisa’, mtoto wake, Sonia George Otieno na mama wa Monalisa, Suzan Lewis ‘Natasha’ walikuwa wakilala hotelini badala ya msibani.
 
Mke wa marehemu (Monalisa) na mwanaye (Sonia) wakiwa katika simanzi katika msiba wa mpendwa wao marehemu George Otieno ‘Tyson’. 

WAREJEA BONGO KIMYAKIMYA BILA KUMZIKA TYSON
Ikazidi kuelezwa kwamba, licha ya kulala hotelini, wiki iliyopita, Mona, mama yake na Sonia walirejea Bongo kimyakimya ili kuendelea na shughuli nyingine za kila siku.
  MKE MWINGINE AZUA BALAA
Wakati ya Monalisa yakiwa hivyo, aliyewahi kuwa mke wa marehemu, Beatrice naye amedaiwa kuzua balaa.
Habari zinadai kwamba, balaa la Beatrice lilianzia jijini Dar ambapo inasemekana baada tu ya kifo cha Tyson, yeye alikwenda nyumbani kwa marehemu na kuzuia kadi ya benki.
“Beatrice alikamata kadi ya benki (ATM) na kusema ana
haki nayo licha ya kwamba hadi anaaga dunia marehemu alikuwa akiishi na mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Lucy.
“Ikatokea kutoelewana kati ya Beatrice na Lucy, Beatrice akawa na kadi lakini hajui password, Lucy anajua. Mwishowe, Beatrice aliamua kumpa kadi ndugu wa Tyson aitwaye Felix Owino,” kilisema chanzo hicho. 
NAYE ALALA KWA NDUGU NAIROBI
Habari kuhusu Beatrice zikaendelea kudai kwamba, naye kama Monalisa, alipofika jijini Nairobi na mwili wa marehemu alikuwa akilala kwa ndugu zake badala ya msibani.
 
Marehemu George Otieno Okumu ‘Tyson’ enzi za uhai wake.
 “Sijajua nini kilitokea msibani kwani baada ya kufika Nairobi na mwili wa marehemu, Beatrice naye akawa analala kwa ndugu zake na si kwenye nyumba iliyofikia msiba,” kilisema chanzo. 
MONALISA AZUNGUMZA NA AMANI
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, juzi Amani lilimsaka Mona kwa njia ya simu ili kujua anasema nini kuhusu mambo yaliyoelekezwa kwake.
KUHUSU KURUDI BONGO
“Ni kweli nimerudi na Sonia na mama. Ilibidi turudi kwa vile Sonia ana mitihani ya darasa la saba wiki ijayo,” alisema Monalisa.
Amani: “Lakini yule si baba yake? Kwa nini asimzike?”
Monalisa: “Nimeshakwambia labda kama una lingine.”
  MADAI YA KULALA HOTELINI
Amani: “Kuna madai kwamba ulipokuwa msibani Kenya, wewe, mtoto na mama yako mlikuwa mkilala hotelini badala ya msibani, ni kweli?”
Monalisa: “Ni kweli.”
Amani: “Kwa nini sasa?”
Monalisa: “Nafasi ilikuwa ndogo, kwa hiyo tulikuwa tunakwenda kulala hotelini, asubuhi tunaenda msibani.”
Amani: “Mona turudi kwenye kitendo cha kurudi Bongo. Kama Sonia ana mitihani, kwa nini asirudi na mama yake wewe ukabaki kusubiri mazishi?”
Monalisa: “Misiba ya kule si kama huku Tanzania, kule siku za misiba ni Jumamosi tu, siku nyingine watu wanaendelea na mambo yao. Sasa na walivyochelewa kuzika sisi wengine huku (Tanzania) tuna kazi za watu (nadhani tenda za filamu) inabidi kurudi ili kuzifanya.” 
BEATRICE, LUCY HAWAKO HEWANI
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, juhudi za kuwatafuta Beatrice na Lucy ziligonga mwamba baada ya simu zao kutokuwa hewani. Wote wapo jijini Nairobi, Kenya wakisubiri kuzika keshokutwa.
 KUHUSU MAREHEMU TYSON
George Tyson alifariki dunia kufuatia ajali mbaya ya gari aina ya Toyota Noah, iliyotokea eneo la Gairo Morogoro. Marehemu na wenzake ambao walijeruhiwa na wanatibiwa mpaka sasa, walikuwa wakitokea Dodoma kwenda Dar.
Mungu ailaze mahali pema peponi. Amina

No comments:

Post a Comment

KATUNI ZA MWAGITO HIZI HAPA MWANANGU.