Wednesday, February 15, 2017

KIBANDAUMIZA: DI MARIA AMZAWADIA MTU KRETI




“NIMESHASEMA Bigi hapa tusikimbiane tu, hawa Piesijii walikuwa kiboko alipokuwapo yule bwana Kadabra lakini tangu ameondoka hamna kitu mle, leo wanakufa tano kweupeee!!”

“Juzi kati kwenye ndiki ya ligi si umeona mtu kafa sita, tena zote zimepigwa kipindi cha pili, sasa kaa hapo uone mchezo na Piesijii ikipata hata bao moja tu umekunywa bia mbili.”
“Bia za nini banah, wewe weka mpunga mezani na mimi niweke, haya tuweke kilo kilo.” 
Ebana eeh, baada ya mabishano kidogo Bigi akagoma kuweka hela kwakuwa aliamini ataila kiulaini lakini akaahidi kumnunulia kreti zima mshikaji wake huyo kama Piesijii itawapiga Baselona.
Wakati Waswazi wale wakitambiana, waomba njaa walikuwa kimya kwakuwa ndiki ilikuwa bado haijaanza lakini baada ya ndiki kuanza ndiyo waomba njaa walipoonekana kuwa walikuwa wengi kuliko Baka wenyewe na kila goli lilipotinga Waswazi walimfuata jamaa na kushangilia mbele yake.
Sasa je, unaambiwa shangwe lilipigwa ile kinomanoma, yaani mwanzo mwenga. Wakuomba njaa walikuwa wakikenua meno na kuagiza hata ambavyo hawakupanga kuagiza.
Kumbe nini, unadhani furaha nayo inapokuwa imezidi kipimo Mswazi mmoja unamkamatia wapi na hasa mfuko wake unapokuwa umetuna kiasi, kama si kwenye kula basi utamkuta kwenye kunywa, yaani hawanaga ubahili inapotokea anacho, noma kweli.
Hii ngoma ilikuwa ni pande za Mbagala ndani ya Kibandaumiza cha Ilulu Stadium, ambacho kipo chini ya Rafael Nachinguru huku kwenye ishu ya uchanjaji akisimama Mohamed Zomboko.
Hapa wanazama Waswazi 100 ingawa siku hiyo haikufikia idadi hiyo ingawa wazee wa ganda la ndizi walikuwa kibao ukiachilia mbali wazamiaji ambao wengi wao walikuwa wakiagiza kinywaji wanavunga kuchanjwa cha mpira.
We jichange unavyoweza mwanakwetu lakini siku ukija pande za Mbagala ndani ya Ilulu Stadium, buku lisikosekane kwa mfuko na hilo litakuruhusu kucheki ndiki moja au mbili ambazo zinapigwa muda mmoja.
Lakini kama nyingine inapigwa wakati mwingine basi itakulazimu kuchanjwa buku jingine, si unajua burudani ya ndiki Uswazi ndiyo kilevi chetu.
Epl ndiyo ligi inayoangaliwa zaidi pande hizi ikifuatiwa na ile ya madafu yaani ligi hii ya marefa na figisu kibwena, ikifuatiwa na La Liga huku nyingine pia zikiwa zinakubalika kimtindo.
Tofauti na maeneo kibao ambayo mzee wa KB amepata kutembelea, kwa mujibu wa Inchaji, huku ukionyesha ndiki usiku mnene imekula kwako.
Waswazi wa huku hawana kawaida hiyo lakini kwa hizi za kuisha sita kasoro wanakuja kiasi kama ilivyokuwa usiku wa Baselona.
Pamoja na kuwa na shangwe za hapa na pale ikiwamo kupuliza vuvuzela, ndani ya Kibandaumiza cha Ilulu kuna amani ya kutosha na hasa wakati linapofungwa goli, ni tofauti na baadhi ya vibandaumiza vingine ambapo mashabiki humwagiana hadi bia, hapa ni wastaarabu ingawa ile kawaida ya kila mmoja kujifanya kocha na huku ipo.
Ebwana eeh, Mbagala ndani ya Ilulu ndiyo pande nilizokuwapo juzi usiku.
Mimi na wewe msomaji tugumiane hapa Alhamisi ijayo lakini kwa wamiliki wa mambo kama hizi nipigieni tu na nitawafikia mwanakwetu.

Kwa video za Kibandaumiza tembelea Mwagito.Tv 

No comments:

Post a Comment

KATUNI ZA MWAGITO HIZI HAPA MWANANGU.